Wakenya watakiwa kujihadhari na mafuriko

Mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha katika maeneo kadhaa ya nchi kati ya Machi 19-24, 2026 na zinaweza kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Martin Mwanje
2 Min Read

Wakenya wametakiwa kuwa macho dhidi ya mafuriko yanayotarajiwa kukumba maeneo kadhaa ya nchi kufuatia mvua kubwa zinazotabiriwa kunyesha katika kipindi cha siku tano zijazo kuanzia leo Alhamisi. 

Kwenye taarifa, Wizara Usalama wa Taifa imewataka Wakenya kuepuka kuendesha magari au kutembea kwenye maji yanayosogea, kuepukana na mafuriko ya rasharasha hata katika maeneo ambako mvua kubwa hazijanyesha, kutojikinga chini ya miti ili kuepuka kupigwa na radi na kuwa waangalifu katika maeneo ambayo yamefahamika kukumbwa na maporomoko ya ardhi kama vile Aberdares na Mlima Kenya.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa (KMD) imetangaza kuwa mvua kubwa zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia leo Alhamisi.

Imesema mvua hizo zinatarajiwa kuongezeka kwa zaidi ya milimita 20 hadi Machi 24.

“Ongezeko la mvua hizo linatarajiwa kufikia kilele kati ya Machi 20-23, 2026, kabla ya kupungua Machi 24,” alisema kaimu Mkurugenzi wa KMD kwenye taarifa.

“Ingawa mvua zinatarajiwa kupungua kuelekea kipindi hiki, zinatarajiwa kuendelea kunyesha katika maeneo kadhaa ya nchi.”

Maeneo ambayo hayo ni eneo la Ziwa Victoria, nyanda za juu magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ufa na nyanda za chini mashariki mwa Bonde la Ufa ikiwemo Nairobi.

Kaunti zinazotarajia kushuhudia mvua kubwa ni pamoja na Turkana, Samburu, Migori, Bungoma, Busia, Kakamega, Vihiga, Pokot Magharibi, Baringo, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia na Nandi.

Zingine ni Uasin Gishu, Nakuru, Siaya, Kisumu, Homa Bay, Kisii, Kericho, Bomet, Kiambu, Embu, Murang’a, Kirinyaga, Nyandarua, Nyeri, Laikipia, Tharaka Nithi, Meru, Nairobi, Narok, Kajiado, Makueni, Machakos, Taita-Taveta, Kitui, Kwale, Mombasa na Garissa.

Maeneo mengine yanayoweza kushuhudia mvua kubwa ni sehemu kadhaa za kaunti za Marsabit, Isiolo, Wajir, Mandera na Tana River.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa inatoa wito kwa wakazi wa maeneo haya kuchukua tahadhari dhidi ya mafuriko yanayoweza kutokea na hali ya kutoweza kuona vizuri.

 

 

Share This Article