Idadi nyingi ya stakabadhi bado hazijachukuliwa na Wakenya katika vituo vingi vya Huduma kote nchini.
Stakabadhi hizo zinajumuisha vitambulisho vya kitaifa na vyeti vya kuzaliwa.
“Kote nchini, kuna zaidi ya vitambulisho vya kitaifa ambavyo bado havijachukuliwa na wenywe, na hapa mjini Thika, kuna zaidi ya vyeti vya kuzaliwa 2,800, zaidi ya vitambulisho 10,000 na leseni za kuendesha magari zaidi ya 6,000 ambazo zinasubiriwa kuchukuliwa na wenyewe,” amesema Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi wakati wa ziara ya ukaguzi wa utendakazi wa kituo cha Huduma mjini Thika, kaunti ya Kiambu leo Alhamisi.
“Ninatoa wito kwa Wakenya wote kuzuru vituo vya Huduma vilivyo karibu nao na kuchukua stakabadhi zao bila kukawia!”
Kuna jumla ya vituo 57 vya Huduma kote nchini.
Muturi amedokeza kuwa kuna mipango ya kuanzisha vituo vya Huduma katika kila eneo bunge ili kuhakikisha raia wanapata huduma bila kusafiri kwa mwendo mrefu.
Muturi akielezea kufurahia hatua ya wabunge kuunga mkono kwa dhati mipango ya kupeleka huduma karibu na raia.