Wakenya wamehimizwa kutochukua sheria mikononi mwao dhidi ya maafisa wa idara ya Mahakama, wanapokosa kuridhishwa na matokeo ya kesi.
Akizungumza leo Jumamosi wakati wa ibada ya mazishi ya Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya Makadara aliyeuawa Monica Kivuti, naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu badala yake aliwataka wakenya kutumia mbinu mbadala za kisheria zilizopo.
“Ikiwa yeyote hajaridhishwa na kazi yetu, msituue. Kumtoa mtu uhai ni kosa la jinai chini ya kifungu cha 203 za sheria za Kenya, na hukumu yake ni kifo chini ya sehemu ya 204 ya sheria za Kenya,” alisema Mwilu.
Philomena alielezea masikitiko yake kwamba maafisa wa mahakama wamekuwa wakikabiliwa na vitisho wanapotekeleza majukumu yao.
“Mbona tufariki tukifanya kazi ambayo tulipewa na Mwenyezi Mungu? Hata tunapokosea msituue, nawasihi,” alieleza naibu huyo Jaji Mkuu.
Aidha, alitoa wito kwa serikali kuhakikisha maafisa wa mahakama wanalindwa na kufanya kazi katika mazingira bora.
Monica Kivuti alifariki wiki jana akipokea matibabu katika hospitali moja Jijini Nairobi, baada ya kupigwa risasi na afisa wa polisi katika Mahakama ya Makadara.
Alizikwa leo Jumamosi katika eneo la Yatta, kaunti ya Machakos.