Wakenya wanaoishi ughaibuni wahimizwa kuwekeza hapa nchini

Tom Mathinji
1 Min Read

Rais William Ruto, amewahimiza wakenya wanaoishi ughaibuni kuwekeza katika miradi ya kilimo, nyumba za gharama nafuu na nguvu kazi humu nchini.

Akiongea leo Jumatano katika jumba la mikutano ya kimataifa la KICC alipofungua rasmi kongamano la pili la kila mwaka kuhusu uwekezaji wa wakenya wanaoishi ughaibuni, Rais alisema serikali inafanya mengi hasa kuwasaidia wakenya hao kuelekeza mawasilisho ya fedha zao humu nchini kwa shughuli zenye faida katika serikali ya kitaifa na zile za kaunti.

Rais Ruto alisema serikali yake inatoa mazingira bora yatakayovutia uwekezaji wa kigeni hapa nchini.

Washiriki katika kongamano la pili la kila mwaka kuhusu uwekezaji wa wakenya wanaoishi ughaibuni, katika jumba la KICC.

Alisema serikali pia itaboresha sera zake ili kufanikisha shughuli za uwekezaji wa wakenya wanaoishi ng’ambo.

Alisema teknolojia ya habari na mawasiliano, utayarishaji ngozi, uchukuzi, kawi safi, nyumba, uchumi wa shughuli za baharini na kilimo ni miongoni mwa fursa za uwekezaji hapa nchini.

Kongamano hilo la siku tatu linanuiwa kuangazia na kutoa fursa za uwekezaji katika nyanja mbali mbali za uchumi kwa wakenya wanoishi ughaibuni, huku wakishauriana kuhusu mikakati ya kisheria na kiusimamizi kuhusiana na uwekezaji huo.

TAGGED:
Share This Article