Huku ongezeko la magonjwa ya kuambukizwa na yasiyo ya kuambukizwa likiendelea kushuhudiwa nchini, wakenya wamehimizwa kukumbatia bima za afya ili kuepuka michango ya kila mara ya kugharamia matibabu.
Akizungumza mjini Meru baada ya kufungua tawi la kampuni ya bima ya afya ya AAR, mkurugenzi mtendaji wa AAR Patrick Gitonga alisema magonjwa kama saratani yamesababisha familia nyingi kusalia masikini baada ya kutumia fedha nyingi kwa matibabu.
Gitonga anatoa wito kwa wakenya kukumbatia hulka ya kuwa na bima ya afya kama njia ya kuhakikisha wanapata usaidizi faafu kila wanapokuwa wagonjwa.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa kaunti ya Meru Joshua Mungania alisema kwamba bima ya afya ni muhimu kwani inaepushia familia mzigo wa kuandaa mchango ili kulipa ada za hospitali.
Alishangaa jinsi wakenya wanaweza kuchukulia mali yao kama magari bima lakini wanakosa kujichukulia bima ya afya.
Meneja wa AAR tawi la Meru Kendi Kimathi, alisema takwimu zinaonyesha kwamba kaunti ya Meru inaongoza kwa visa vya ugonjwa wa saratani huku akiomba watu wa eneo hilo kuchukua bima ya afya.
Kulingana na Kendi kampuni yao ya AAR inajazilia juhudi za serikali chini ya mpango wa huduma bora za afya kwa wote kwa kutoa bima za bei nafuu ambazo hazina kikwazo cha umri kwani wanaweza hata kusajili mtu wa miaka 100.