Wakenya wahakikishiwa usalama kutokana na ugonjwa wa Mpox

Marion Bosire
2 Min Read

Katibu wa afya ya umma Mary Muthoni amehakikishia wakenya kwamba serikali imeweka mikakati kabambe kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Mpox humu nchini.

Muthoni anasema serikali iko makini kabisa kuhakikisha kwamba kila kisa cha ugonjwa huo nchini kinashughulikiwa haraka na hivyo hakuna haja ya hofu huku mkurupuko wa ugonjwa huo ukiripotiwa katika eneo la mashariki la bara Afrika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni iitwayo, “Epuka Uchafu Afya Nyumbani” huko Kapenguria, Muthoni alisema wizara ya afya imekuwa ikishughulika vilivyo na kila kisa cha ugonjwa huo kimesimamiwa ipasavyo.

Kufikia sasa ni visa viwili pekee vya ugonjwa wa Mpox vimethibitishwa nchini ambapo mmoja wa wagonjwa hao ametibiwa na kuruhusiwa kurejea kwenye nchi yake.

Kulingana na Muthoni waendeshaji wa magari makubwa ya mizigo wanaozuru nchi mbali mbali kikazi wapatao 400 wamepimwa ogonjwa wa Mpoz katika vituo mbali mbali vya mpakani.

Aliongeza kwamba Kenya haina visa vingi vya ugonjwa wa Mpox lakini ni lazima isalie macho kwa sababu ya nchi jirani ambazo wananchi wake huzuru nchi nyingine mara kwa mara hasa waendeshaji hao wa magari ya mizigo.

Katibu Muthoni alifafanua kwamba ugonjwa wa Mpox ni tofauti na ugonjwa wa Covid-19, hata ingawa unaambukiwa kwa njia sawa ambayo ni kutangamana na mgonjwa.

Shirika la afya ulimwenguni lilielezea kwamba virusi vya ugonjwa wa Mpox husambaa kwa kukaribia aliyenavyo hasa kwa kuguzanisha ngozi, midomo au midomo na ngozi.

Tofauti na Covid 19, wakenya hawatalazimika kuvaa barakoa wakati huu wa Mpox.

Share This Article