Wakenya waandamana kupinga Mswada wa Fedha 2024

Martin Mwanje
1 Min Read

Baadhi ya Wakenya leo Jumanne walifanya maandamano jijini Nairobi kupinga Mswada wa Fedha 2024. 

Hii ni licha ya serikali kutangaza kuondolewa kwa mapendekezo tata kwenye mswada huo ambayo wanasema yangefanya gharama ya maisha kuwa kupanda hata zaidi.

Usalama uliimarishwa nje ya majengo ya bunge huku polisi wakirusha vitoza machozi kutawanya baadhi ya waandamanaji.

Akiwahutubia wanahabari baada ya mkutano wa wabunge wa Kenya Kwanza katika Ikulu ya Nairobi, mwenyekiti wa kamati ya fedha Kuria Kimani alitangaza kuwa mapendekezo kadhaa yaliyopingwa na Wakenya yameondolewa kwenye mswada huo.

Hii ni pamoja na mpango wa kutoza ushuru bidhaa kama vile mkate na magari.

Ushuru mwingine ambao umetolewa kwenye mswada huo ni pamoja na ushuru wa asilimia 2.5 wa magari, ushuru wa usafirishaji wa sukari, ushuru wa mafuta ya kupikia, ushuru wa kubadilisha sarafu na wa huduma nyingine za kifedha.

Kuria pia alitangaza kwamba gharama ya kutuma pesa kupitia rununu pia haitaongezeka ilivyopendekezwa awali.

Hata hivyo, Wakenya wanasema mswada huo unapaswa kukataliwa bungeni kwani huenda una kodi zingine fiche ambazo zitafanya gharama ya maisha kupanda.

Wakati wa maandamano hayo, Wakenya walioandamana walibeba mabango yaliyoelezea baadhi ya mapendekezo wanayoyapinga.

Mswada wa Fedha 2024 utawasilishwa bungeni leo Jumanne.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *