Wakenya watapata fursa adimu ya kuingia bila malipo katika mbuga za wanyama za kitaifa zinazosimamiwa na Shirika la Wanyamapori nchini, KWS Jumamosi hii, Septemba 27.
Hatua hiyo imechukuliwa na serikali ili kuwapa Wakenya fursa ya kuungana na dunia nzima katika kuadhimisha Siku ya Utalii Duniani ya Umoja wa Mataifa.
“Ili kuheshimu siku hii muhimu, nimefurahia kutangaza kwamba serikali ya Kenya inawakubalia raia wote wa Kenya kuingia bila malipo katika mbuga za wanyama za kitaifa zinazosimamiwa na Shirika la Wanyamapori nchini, KWS siku ya Jumamosi, Septemba 27, 2025,” alisema Waziri wa Utalii Rebecca Miano kwenye taarifa.
“Hatua hii ni fursa kwa kila Mkenya kujionea wanyamapori wetu wanaopendeza, kuimarisha dhamira yetu ya pamoja ya uhifadhi, na kushuhudia uzuri usiolinganishwa na chochote wa hazina zetu asili.”
Waziri akiongeza kuwa lengo la kuwakubalia Wakenya kutembelea mbuga hizo ni kuwapa fursa ya kutambua utajiri wa uhaianuwai wa nchi hii na kutia moyo uwajibikaji wa pamoja wa kuutunza.
“Tunawaalika Wakenya wote kutumia fursa hii kujionea, kujifunza na kusherehekea maajabu ya mbuga zetu, ambazo siyo tu fahari ya Kenya lakini pia urithi wa dunia,” aliongeza Waziri wa Miano.
Kaulimbiu ya Siku ya Utalii Duniani mwaka huu ni “Utalii na Maendeleo Endelevu.”