Wakenya 2 washtakiwa kwa kusaidia kuingiza Waeritrea 30 humu nchini

Wako Ali
1 Min Read

Wakenya wawili wameshtakiwa katika mahakama ya Marsabit kwa kosa la kusaidia kuwaingiza humu nchini kinyume cha sheria wahamiaji haramu 30 raia wa Eritrea.

Stephen Obocha mwenye umri wa miaka 26 na Ahmed Mohamed wa miaka 24 wanakabiliwa na kosa hilo wanalodaiwa kulitekeleza Machi 15 mwaka huu katika eneo la Illeret, kaunti ndogo ya Horr Kasikazini, gatuzi la Marsabit.

Kulingana na mashtaka dhidi yao, Obocha na mwenzake, wote wakazi wa Lokesheni ya Hula Hula waliwasaidia wahamiaji hao haramu kusafirishwa kutoka taifa jirani la Ethiopia hadi humu nchini bila stakabadhi zozote halali.

Wanadaiwa kutumia gari aina ya Nissan Patrol lenye nambari ya usajili, EXGKB 997R kuingia humu nchini kinyume cha sheria.

Hata hivyo, walipofikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi wa mahakama ya Marsabit Simon Arome, wote wawili walikanusha mashtaka dhidi yao.

Mahakama imewaachilia kwa dhamana ya shilingi milioni 5 kila mmoja.

Kesi hiyo itatajwa tarehe 2 mwezi ujao.

Wako Ali
+ posts
Share This Article