Vijiji kadhaa mjini Voi vimezingirwa na mafuriko baada ya mto Voi kuvunja kingo zake leo Jumatatu asubuhi.
Shirika la Msalaba Mwekundu limeanzisha zoezi la utafutaji na uokozi wa wakazi ambao nyumba zao zimefurika maji.
Katika video moja iliyopachikwa na shirika hilo katika mtandao wa X, baadhi ya wanafamilia wanaonekana wakiwa wamepanda hadi juu ya paa kukimbilia usalama wao.
Kwa upande mwingine, maafisa wa shirika hilo wanaonekana wakiwaokoa watoto kutoka kwa baadhi ya nyumba.
Ongoing rescue in Voi after the Voi River burst its banks this morning. https://t.co/v2imE4eQ8F pic.twitter.com/MGoyXz8FDY
— Kenya Red Cross (@KenyaRedCross) December 4, 2023
Kule Migori, Shirika la Msalaba Mwekundu limeripoti kuzama kwa boti katika mto Migori katika eneo la Matanda.
Watu watano waliokuwa kwenye boti hiyo waliokolewa kutokana na hatua za haraka zilizochukuliwa na maafisa wa shirika hilo wakisaidiwa na wakazi wa eneo hilo.
Hata hivyo, mtu mmoja bado hajapatikana.
Shirika la Msalaba Mwekundu kwa kushirikiana na serikali ya kaunti zimeongeza idadi wapiga mbizi katika juhudi za kumtafuta mtu huyo.