Wakazi zaidi ya 300 wa kaunti ya Meru na maeneo ya karibu walinufaika na huduma za bure za kimatibabu kufuatia kuandaliwa kwa kambi ya matibabu bila malipo na chuo kikuu cha Kenya Methodist University – KeMU, hususan kitivo cha Afya.
Serikali ya kaunti ya Meru na wahisani wengine pia walihusika na maandalizi ya kambi hiyo.
Daktari Eliaps Some, naibu chansela wa chuo kikuu cha KeMU alielezea kwamba kambi hiyo ya siku tatu iliyoanza jana inalenga kusaidia watu ambao hawawezi kumudu huduma za afya katika hospitali za kibinafsi na hata za umma.
Some alifafanua pia kwamba chuo hicho hufanya hivyo kila mwaka kama njia ya kuisaidia jamii.
Huku akitoa wito kwa wakazi kutumia fursa ya kambi hiyo kupata matibabu, Some alisema madaktari wanaohudumu huko ni wa hospitali ya Meru level 5 na wa hospitali nyingine zilizo karibu.
Baadhi ya huduma zinazotolewa humo ni vipimo vya sukari, vya mapigo ya damu, vya saratani kati ya nyingine nyingi na wagonjwa wanaohitaji rufaa wanaelekezwa katika hospitali mbali mbali ikiwemo Meru level 5.
Afisa anayesimamia masuala ya afya katika serikali ya kaunti ya Meru Joseph Wahome alisema wataendelea kushirikiana na chuo cha KeMU kwa manufaa ya wakazi wa eneo hilo.
Mmoja wa waliofaidika alipongeza walioandaa kambi hiyo na kuwahimiza kuendelea hivyo.