Takriban wajumbe 30,000 watahudhuria Mkutano wa Tabia Nchi wa Afrika uliopangwa kuandaliwa jijini Nairobi mwezi ujao.
Mkutano huo utafanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la Kenyatta, KICC kati ya Septemba 4 na 6, 2023.
Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya kufanyika kwa mkutano wa Baraza la Mawaziri ulioandaliwa katika Ikulu Ndogo ya Kakamega leo Jumanne na kuongozwa na Rais William Ruto.
“Katika kuthibitisha uongozi wa Kenya duniani katika mabadiliko ya tabia nchi, Baraza la Mawaziri lilielezea kuwa Mkutano wa Tabia Nchi wa Afrika ambao umepangwa kuandaliwa jijini Nairobi umevutia nadhari kubwa ya dunia,” ilisema taarifa iliyotolewa baada ya kufanyika kwa mkutano wa Baraza la Mawaziri.
“Mkutano huo utakaofanyika kuanzia Septemba 4 hadi 6, 2023 utahudhuriwa na zaidi ya Wakuu wa Nchi na Serikali 20, wawakilishi wa ngazi za juu wa washirika wa kimaendeleo na taasisi za kimataifa na pia wataalam wa masuala ya tabia nchi; huku idadi ya wajumbe ikitarajiwa kuwa takriban 30,000.”
Baraza la Mawaziri likielezea kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaendelea kuwa tishio kwa usalama na uthabiti wa siku zijazo za nchi hii.
Kulingana na baraza hilo, hali hiyo inachangiwa na uhaba wa malisho ya mifugo, maji na rasilimali zingine asilia.
Kutokana na ukweli huo, Baraza la Mawaziri limeelekeza kuwa kuanzia sasa, mabadiliko ya tabia nchi yatakuwa sehemu ya mipango yote ya kimkakati ya kitaifa.