Wajane kaunti ya Kilifi wataka serikali kupiga jeki miradi yao

Tom Mathinji
1 Min Read

Baadhi ya wajane pamoja na wanawake wa familia za mzazi mmoja eneo la sabaki kaunti ya kilifi, sasa wanaitaka serikali kuu pamoja na ile ya kaunti ya kilifi kuwapiga jeki kwenye miradi yao ili kuinua maisha yao baada ya kusambaratika.

Akina mama hao takriban 100 wanasema kuwa wameanzisha miradi midogo midogo ili kujiendeleza ila changamoto ni kukosa fedha za kuinua miradi yao huku lindi la unaskini miongoni mwao likiendelea kuwakodolea macho kila uchao.

Wakiongozwa na Josphine Masha mmoja wa akina hao anasema kuwa baadhi yao wanategewa na watoto wao ambao kwa sasa baadhi yao wameshindwa kwenda shule kutokana na ukosefu wa Karo.

Marium Juma vile vile anasema kuwa kuna haja ya serikali kipitia viongozi kuwapiga jeki akina mama hao ambao wameonyesha ari ya kujiendeleza japo wamekua wakitegemea wasamaria wema katika juhudi zao za kujiendeleza.

Mwakilishi wa wadi katika eneo hilo Rose Baraka amewahimiza akina mama hao kuendelea kujiunda kimakundi ili waweze kufaidi miradi ambayo imeanzishwa na kaunti ya kilifi.

Mmoja wa wafadhili waliojitokeza Nadia Carlini pamoja na Julius Mweni kwa kauli moja wamesistiza haja ya serikali kuwatambua wajane ambao wanapitia changamoto za kifamilia kuinua biashara zao sambamba na miradi yao ya kujiendeleza.

TAGGED:
Share This Article