Gavana wa zamani wa kaunti ya Kiambu Ferdinand Waititu amehukumiwa kifungo cha miaka 12 jela katika kesi ya utoaji zabuni kinyume cha sheria ya shilingi milioni 588 iliyomkabili yeye, mkewe na watu wengine watano.
Hata hivyo, Waititu anaweza akakwepa kifungo hicho ikiwa atalipa faini ya shilingi milioni 53.5.
Katika kutoa hukumu hiyo, Hakimu Mkuu Thomas Nzioki amesema alifuata miongozo ya utoaji hukumu ikizingatiwa Waititu alinufaika na hongo ya shilingi milioni 25.5 katika utoaji wa zabuni hiyo.
Mkewe Waititu, Susan Wangare amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela ikiwa atakosa kulipa faini ya shilingi laki tano.
Mshtakiwa wa nne, Charles Chege ambaye alikuwa Mkurugenzi wa kampuni ya Testimony iliyohusika katika zabuni hiyo ndio aliyetozwa faini ya juu zaidi baada ya kutakiwa kulipa shilingi milioni 294.5.
Hakimu Nzioki alimwonya Chege dhidi ya kujiingiza katika makubaliano ya kibiashara bila kufuata taratibu za ununuzi bila kufuata sheria.
Jana Jumatano, mahakama iliwapata Waititu na mkewe na hatia katika mashtaka 9 kati ya 12 yaliyowasilishwa mahakamani dhidi yao.
Baadhi ya mashtaka yaliyowakabili ni pamoja na ufisadi, ukinzani wa maslahi, ulanguzi wa pesa, utumizi mbaya wa mamlaka na kujihusisha na mali ya kutiliwa shaka, miongoni mwa mengine.
Kulingana na Hakimu Mkuu, upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa kutosha kudhihirisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.
Hata hivyo, mahakama hiyo iliwaondolea mashtaka matatu yaliyohusiana na utakatishaji wa fedha.