Viongozi wa dini ya kiisilamu katika mji wa Jinja nchini Uganda wanataka awamu ijayo ya tamasha ya muziki ya Nyege Nyege itupiliwe mbali kwa sababu inakiuka maadili.
Tamasha hiyo ambayo huandaliwa kila mwaka, imepangiwa kuanza Novemba 9, 2023 jijini Jinja. Kiingilio ni shilingi elfu 120 pesa za Uganda kwa kila mmoja kila siku na itaendelea kwa muda wa siku tatu.
Khadi wa wilaya ya Jinja Sheikh Ismail Basoga Adi, amesema kwamba hata ingawa tamasha hiyo itawaletea wengi mapato, dini haikubaliani nayo.
Alisema kwamba mambo ambayo hufanyika katika tamasha ya Nyege Nyege sio mazuri hasa kwa vijana wa umri mdogo.
Basoga alitoa maoni hayo alipohutubu kwenye hafla ya kuchangisha pesa za kusaidia kundi la kina mama waisilamu wa eneo la Busoga jijini Jinja.
Mmoja wa waandalizi wa yamasha ya Nyege Nyege Derick Debru, kutoka Talent Africa, alisema mwezi jana kwenye mahojiano kwamba chimbuko la mto Nile, uwanja wa maonyesho wa Jinja, hoteli ya Source Garden, bustani ya Nile na sehemu ya uwanja wa gofu ndiyo maeneo atakayotumiwa kuandaa awamu ya mwaka huu ya tamasha hiyo.
Waziri wa utalii katika ufalme wa Busoga Hellen Namutamba, alisema wameamua kuunga mkono maandalizi ya tamasha hiyo jijini Jinja kwa sababu inaleta mengi mazuri kama mabanda ya kuonyesha utamaduni wa watu wa eneo hilo.
Utetezi wa wawili hao unafuatia hatua ya Sheikh Ismail Basoga Adi ya kushangaa ni kwa nini zamu hii, tamasha hiyo inaandaliwa katikati ya jiji ilhali awali iliandaliwa katika sehemu nyingine.
Hii sio mara ya kwanza tamasha ya Nyege Nyege inaangaziwa, mwaka jana spika wa bunge la Uganda Anita Among, alielekeza kwamba itupiliwe mbali kwa sababu ilikuwa inatoa fursa ya ukiukaji wa maadili ya jamii.
Kuna viongozi wengine hata hivyo wanaunga mkono maandalizi ya tamasha hiyo akiwemo waziri wa masuala ya Afrika mashariki nchini Uganda Rebecca Kadaga na kamishna mkazi wa Jinja Darius Nandinda.