Madaktari wanagenzi leo Jumatatu walikita kambi nje ya ofisi za Wizara ya Afya na kuitaka serikali kuharakisha mchakato wa kuwatuma kuhudumu katika hospitali mbalimbali nchini kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano, CBA wa mwaka 2017.
Chama cha Madkatrai nchini, KMPDU kupitia kwa Katibu wao Davji Atellah kimeapa kuishinikiza serikali kuwapatia madaktari hao barua za kuanza uanagenzi wao uliocheleweshwa mno chini ya mkataba huo.
Ikiwa hilo shinikizo zao zitafuta dafu, basi kila mwanagenzi atapokea malipo ya shilingi 206,000 kila mwezi kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uanagenzi kinyume cha shilingi 70,000 zinazopendekezwa na serikali.
Dkt. Atellah amesema kwamba serikali bado haijatekeleza makubaliano yaliyoafikiwa kati yao na serikali na kusababisha kukomeshwa kwa mgomo wao mwanzo wa mwezi Mei mwaka huu.
Madaktari hao wanagenzi walikita kambi nje ya ofisi za Wizara ya Afya saa chache tu baada ya tangazo kwenye akaunti ya KMPDU ya mtandao wa X kusema kwamba walikuwa wamesimamisha mipango ya kugoma nje ya jumba la Afya jijini Nairobi.
Lakini Dkt. Atellah amefafanua kwamba akaunti ya X ya chama chao cha KMPDU imedukuliwa akiongeza kusema kwamba wataendelea kuwasilisha malalamishi yao hadi pale ambapo matakwa yao yatatekelezwa.
Mojawapo ya matakwa yao ni kutumwa kwa madaktari wanagenzi kwenye hospitali mbalimbali za umma nchini, kama ilivyoafikiwa kwenye mkataba wa makubaliano ya pamoja wa mwaka 2017.
Madaktari walimaliza mgomo wao wa siku 56 mwezi Mei mwaka huu baada ya majadiliano ya siku kadhaa ambapo mwishowe waliafikia makubaliano na serikali.