Naibu Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa Mawaziri kutekeleza ajenda ya maendeleo ya Kenya Kwanza, ili kuhakikisha taifa hili linapiga hatua za kimaendeleo.
Akizungumza alipofunga mkutano wa siku mbili wa uhamasisho wa Baraza la Mawaziri mtaani Karen, Nairobi, Gachagua alisema mkutano huo umewapa viongozi hao nguvu mpya kutekeleza ajenda za maendeleo kwa wakenya.
“Mkutano huu wa uhamasisho ulioandaliwa na Rais William Ruto, umeweka mikakati ya kutekelezwa kikamilifu kwa mipango ya Kenya Kwanza ya kubadilisha taifa hili.
Naibu huyo wa Rais aliwakumbusha Mawaziri hao kwamba heshima kubwa kuhudumu katika Baraza la Mawaziri, huku akiwataka viongozi hao kujibidiisha zaidi katika utoaji wa huduma.
Mkutano huo wa uhamasisho ulijiri baada ya Rais William Ruto kubuni Baraza jumuishi la Mawaziri, akisema litaunganisha wakenya wote na kushughulikia maswala yaliyoibuliwa wakati wa maandamano dhidi ya serikali.