Wahandisi wa matibabu wataka serikali idhibiti sekta hiyo

Dismas Otuke
2 Min Read

Chama cha wahandisi wa matibabu nchini AMEK, kimeitaka wizara ya afya kuingilia kati na kuharakisha kubuniwa kwa shirika la kudhibiti watalaam hao wa mitambo inayotumika hospitalini.

Wakizungumza jana wakati wa kuapishwa kwa maafisa wapya waliochaguliwa wa chama hicho, walisema sekta hiyo imeingiliwa na wahandisi ambao hawajasajiliwa wanaokarabati mitambo ya hospitalini na kuhatarisha maisha ya wagonjwa.

Katibu mratibu wa AMEK Millicent Alooh alisema idadi ya wahandisi ghushi wanaokarabati mashine za hospitalini imeongezeka, na ipo haja ya kuharakishwa  kubuniwa kwa chama cha kudhibiti shughuli zao, hali ambayo pia itasaidia kupunguza hasara kwa hospitali za umma na zile za kaunti kutokana na kuharibika mara kwa mara kwa mashine .

Aidha Alooh alisema kuna idadi kubwa ya wahandisi wanaofuzu kila mwaka, lakini hawapati ajira, na ni kupitia tu kubuniwa kwa shirika la kudhibiti ambapo wengi wao watapata ajira.

Upande wake Mwenyekiti wa AMEK, Symon Mbakah, alimtaka Katibu mpya wa Huduma za Matibabu, Dkt Ouma Oluga, kuharakisha mchakato wa kubuniwa kwa chama cha kudhibiti wahandisi na kushinikiza kuongezwa kwa idadi ya wahandisi wanaohudumu katika hospitali za umma na zile za kaunti.

Symon Mbakah alihifadhi kiti cha Mwenyekiti wa AMEK huku Hesborne Obaigwa, akichaguliwa Katibu Mkuu kuchukua nafasi ya Millicent Alooh, ambaye ndiye Katibu Mratibu mpya.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *