Watu wasiojulikana Jumatatu usiku, walimdunga kisu mara kadhaa na kumuua mhudumu wa bodaboda, katika eneo la Arobota , eneo bunge la Saku kaunti ya Marsabit.
Marehemu ambaye alikuwa na umri wa makamu na aliyehudumu katika eneo la 44 mjini Marsabit, alihadaiwa na watu wasiojulikana waliojisingizia kuwa wateja.
Huku akimshukuru Mungu kwa kumpa wateja, mwathiriwa huyo aliwabeba wateja hao bila kujua mauti yalikuwa yakimsubiri huko mbele.
Baada ya mwendo usio mrefu, abiria hao walimgeukia mwathiriwa na kumshambulia kutumia kisu.
Baada ya kutekeleza unyama huo, wahalifu hao walitoroka kutumia pikipiki ya mwathiriwa, huku maafisa wa polisi wakianzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Marsabit kusubiri kufanyiwa upasuaji.