Wafungwa katika magereza ya Kenya wana kila sababu ya kutabasamu kwani sasa wanaweza kupata fursa ya kuhudhuria mazishi ya wapendwa wao.
Hili litawezekana tu kwa wale ambao hawana kikwazo chochote kitakacholazimu usimamizi wa magereza kuwanyima haki hiyo.
Haya yanatokana na kesi iliyowasilishwa mahakamani na mwanahabari Moses Dola ambaye anatumikia kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kosa la kuua mke wake.
Aliamua kuwasilisha kesi hiyo baada ya kukosa kuhudhuria mazishi ya mamake mzazi akitaja hatua ya kumnyima fursa ya kwenda kuzika mamake kuwa hujuma kwa wafungwa.
Kulingana naye, hatua hiyo pia ni ukiukaji wa haki za msingi za wafungwa pamoja na uhuru wao.
Dola alihukumiwa kifungo hicho mwaka 2018 na mamake mzazi aliaga dunia Julai 12, 2021.
Jaji Lawrence Mugambi wa mahakama kuu nchini alisema kwamba wafungwa wana haki ya kuhudumiwa kama binadamu wengine.
Hata hivyo alisema kwamba mahakama haiwezi kusahau usalama wa watu watakaokuwa kwenye hafla kama hizo na hivyo basi usalama huo utaangaziwa katika kuwapa wafungwa fursa kuhudhuria mazishi ya wapendwa wao.
Mahakama wakati wa kutoa uamuzi wake kwenye kesi hiyo iliamuru serikali kuandaa taratibu zitakazotumiwa kuamua wafungwa ambao hawatapatiwa fursa ya kwenda kuzika wapendwa wao.
Serikali ina muda wa miezi sita kuwasilisha orodha ya taratibu hizo.