Wafuasi wawili wa Alshabab wafariki wakitega vilipuzi barabarani

Tom Mathinji
1 Min Read

Washukiwa wawili wa kundi la wanamgambo wa Al-Shabab, walifariki baada ya kulipuka kwa kilipuzi cha kutegwa ardhini katika kaunti ya Garissa.

Kulingana na taarifa ya maafisa wa polisi wa kitengo cha DCI, kifaa hicho kililipuka Jumanne asubuhi, wanamgambo wa Al-Shabaab walipokuwa wakikitega ardhini katika barabara moja kaunti ya Garissa na kuwaua wawili papo hapo huku wengine wakitoroka na majeraha mabaya.

“Kundi la wafuasi wa Al-Shabaab lilikuwa likitega kilipuzi katika barabara moja kaunti ya Garissa, hata hivyo kililipuka na kuwaua wenzao wawili papo hapo huku wengine wakitoroka na majeraha,” ilisema DCI kupitia mtandao wa twitter.

Wanamgambo hao wamekuwa wakitega vilipuzi barabarani katika eneo hilo, huku wakilenga maafisa wa usalama wanaoshika doria. Maafisa kadhaa wameangamia kutokana na vilipuzi hivyo

Maafisa wa kushika doria mpakani walifika katika eneo la mkasa katika barabara ya Amuma-Ruqa, na kuthibitisha kisa hicho.

Maafisa hao wa polisi walisema mlipuko huo ulikuwa na kishindo kikubwa, huku sehemu za miili za wanamgambo hao zikitapakaa katika sehemu ya mkasa.

DCI ilisema maafisa hao walianzisha msako katika eneo hilo kuwasaka wanamgambo waliotoroka.

TAGGED:
Share This Article