Vuta nikuvute ilishuhudiwa leo Ijumaa, wakati wafuasi wa Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula walipokabiliana katika hafla ya mazishi.
Wafuasi wa wanasiasa hao walikabiliana kwa mawe eneo la Goseta Kaunti ya Trans Nzoia.
Wetangula na Natembeya walikuwa wamehudhuria hafla hiyo.
Sintofahamu hiyo inaaminika kutokana na kufurushwa kwa wakazi kutoka kwa ardhi moja ya ekari 2,700, inayoaminika kumilikiwa na Magereza ya mjini Kitale Kaunti ya Trans Nzoia.
Natembeya analaumiwa kwa kuunga mkono amri ya Rais William Ruto ya kuwafurusha wakazi hao katika ardhi hiyo.
Gavana huyo amejipata matatani kutoka kwa viongozi wa Kenya Kwanza hususan Spika Wetangula. Spika huyo anamlaumu Natembeya kwa kuchochea kufurushwa kwa watu hao.
Natembeya alijitetea kwa kusema kuwa agizo la kufurushwa kwa watu hao lilitolewa na Rais wala hausiki kamwe.
Alikanusha kupata faida zozote za kibinafsi kutokana na mzozo wa ardhi hiyo, akitetea hitaji la kujenga nyumba za bei nafuu.