Wafanyakazi 79 wa serikali ya kaunti ya Nyamira wasimamishwa kazi

Tom Mathinji
2 Min Read
Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo akiwahutubia wanahabari.

Wafanyakazi 79 wa serikali ya kaunti ya Nyamira wamesimamishwa kazi, kwa madai ya kutumia hati ghushi za masomo kupata ajira.

Gavana wa kaunti hiyo Amos Nyaribo, alisema wafanyakazi hao 79 walipatikana na hati ghushi baada ya kaunti hiyo kuwasilisha hati za wafanyakazi 2,821 kuthibitishwa na baraza la kitaifa la mitihani nchini, (KNEC) na vyuo.

Kulingana na Gavana huyo, idara zilizoathiriwa katika serikali hiyo ni pamoja na idara ya Afya wafanyakazi 24, ile ya fedha na utumishi wa umma, wafanyakazi 13 kila moja, afisi ya Gavana na idara ya ardhi wafanyakazi tisa kila moja, idara ya elimu na mazingira wafanyakazi watatu kila moja, idara za jinsia, biashara na bodi ya utumishi wa umma mfanyakazi mmoja kila idara.

Alisema kuwa mishahara ya wafanyakazi hao imesimamisha, huku hatua za kinidhamu dhdi yao zikianzishwa.

Aidha Nyaribo alisema serikali yake itawasilisha ripoti kuhusu visa hivyo kwa idara ya upelelezi wa maswala ya jinai na tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi EACC.

Alidokeza kuwa serikali yake itawasilisha hati za kundi la pili la wafanyakazi juma lijalo, akisema kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya watu waliopandishwa vyeo kwa njia isiyofaa.

“Nawahakikishia wakazi wa kaunti ya Nyamira kuwa zoezi hilo linalenga kuimarisha utumishi wa umma wa kaunti hiyo, ili kuboresha utoaji huduma kwa wakazi,” alisema Gavana Nyaribo.

Share This Article