Mamlaka ya kitaifa ya uchukuzi na usalama barabarani NTSA imesema kwamba waendesha pikipiki za uchukuzi wa abiria almaarufu boda boda na wanaotembea kwa miguu ndio wahasiriwa wakuu wa ajali za barabarani mwaka huu.
Kulingana na ripoti ya NTSA, watu 4,282 waliuawa kwenye ajali za barabarani kufikia Novemba 2024. Kati ya wahasiriwa hao, 1600 ni watu waliokuwa wakitembea kwa miguu huku 900 wakiwa waendesha boda boda.
Meneja msaidizi wa NTSA katika eneo la Pwani John Parteroi amesema kwamba wameanzisha kampeni ya kuhamasisha wote wanaotumia barabara katika eneo hilo hasa msimu huu wa sherehe.
Kampeni hiyo iliyoanzishwa Disemba 10, 2024 inalenga madereva, wanaokwenda kwa miguu na waendesha boda boda huku madereva wa magari ya uchukuzi wa abiria wakitia saini azimio la kuwa waangalifu barabarani.
Parteroi alisema wanaelimisha watumizi wa barabara kuhusu usalama barabarani kwa kuzingatia sheria za trafiki msimu huu wa sherehe.
Wanaokwenda kwa miguu wanashauriwa kutumia mapito ya juu kwa juu kuvuka barabara badala ya kuvuka barabara zenye shughuli nyingi na kuhusika kwenye ajali.
Eneo la Kijipwa kwenye barabara kuu ya kutoka Kilifi kuelekea Malindi limetajwa kuwa lenye hatari kubwa kwani waendeshaji magari huendesha kwa kasi ya juu mno.