Wadhibiti wa dawa za wadudu wafanya uchunguzi Lamu

Marion Bosire
1 Min Read

Bodi ya kitaifa ya kudhibiti dawa za kuua wadudu shambani imieanzisha uchunguzi kuhusu matumizi mabaya ya dawa hizo katika eneo la Mpeketoni, kaunti ndogo ya Lamu Magharibi, kaunti ya Lamu.

Lengo la uchunguzi huo ni kubainiiwapo wakulima wanatumia dawa za kuua wadudu kulingana na viwango vinavyokubaliwa.

Fredrick Muchiri anayeongoza uchunguzi huo alisema kwamba watakusanya sampuli za mimea kutoka sehemu mbali mbali za kaunti ya Lamu kwa uchunguzi zaidi katika maabara ya serikali.

Alisisitiza kwamba hatua yao inalenga kuchunguza iwapo kemikali zinazotumiwa kuua wadudu shambani zinaafiki viwango vya usalama vilivyowekwa.

Kando na uchunguzi huo, bodi hiyo ya kudhibiti matumizi ya dawa za wadudu itaendelea kuwapa wakulima mafunzo kote nchini.

Mafunzo hayo yanalenga kuwapa wakulima ujuzi kuhusu umuhimu wa kutumia kemikali zilizoidhinishwa na serikali ili kuepuka hatari za kiafya na kimazingira.

Waziri wa kilimo katika serikali ya kaunti ya Lamu James Gichu, amesema kwamba visa kadhaa kuhusu matumizi mabaya ya dawa za kuua wadudu vimeripotiwa katika muda wa miezi michache iliyopita.

Hata hivyo anatambua kwamba idara ya kilimo ya kaunti imeweza kushughulikia visa hivyo huku ikijitahidi kuvitatua.

Share This Article