Wadau wasaka mikakati ya kupambana na athari za mafuriko

Martin Mwanje
2 Min Read

Athari za mvua za El Nino zinazonyesha katika sehemu nyingi za nchi zinaendelea kushuhudiwa kila uchao.

Mafuriko yaliyotokana na mvua hizo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 70 huku angalau familia 36,000 zikiachwa bila makazi.

Ni hali ambayo imeitia serikali na washhikadau mbalimbali tumbo joto.

Wakati Rais William Ruto akiongoza Baraza la Mawaziri kutafuta mikakati ya kukabiliana na athari za mvua hiyo, washikadau wa afya nao walikuwa kikaoni wakijikuna kichwa juu ya mbinu bora za kuzipiga dafrau athari za mafuriko.

Katika mkutano ulioongozwa na Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni, washikadau hao walikubaliana kuungana kukabiliana na changamoto za kibinadamu na kiafya zinazosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kushuhudiwa nchini.

“Majadiliano ya leo yaliangazia mikakati ya kurejesha miundombinu ya afya, mahitaji muhimu ya afya na kuimarisha uangalizi wa magonjwa,” alisema Katibu Muthoni baada ya mkutano huo.

“Tulibuni mpango madhubuti wa kuratibu rasilimali muhimu.”

Mpango huo ni pamoja na usambazaji wa vyakula vyenye virutubishi muhimu kwa waathiriwa wa mafuriko hayo.

Wadau pia walijadiliana juu ya utoaji wa matibabu ya muda na vituo vya uokozi, wakisisitiza umuhimu wa kuhusisha jamii ipasavyo ili kuhakikisha usalama wake.

Wadau wengi walitoa wito wa kutoa usaidizi wa mara kwa mara kwa waathiriwa wa mafuriko, kuwaondolea mateso, kuokoa maisha na kuharakisha urejeshwaji wa huduma za matibabu katika kaunti zilizoathiriwa zaidi na mafuriko.

Mombasa, Mandera, Wajir, Isiolo na kimsingi kaunti za kaskazini mashariki mwa nchi zimeathiriwa mno na mafuriko, hali ambayo imekatiza usafiri, utoaji huduma za matibabu na wakazi wengi kukosa chakula.

Share This Article