Shule ya msingi ya Nataparkakono, iliyoko kwenye mpaka wa eneo bunge la Turkana ya Kati na Loima, kwa sasa ipo katika hali ya hatari kufuatia kuporomoka kwa darasa moja la shule hiyo.
Hali hii imezua hofu kubwa miongoni mwa wazazi, walimu, na wanafunzi, hasa ikizingatiwa kuwa madarasa mengine yaliyosalia pia yana mianya na nyufa zinazoashiria uwezekano wa kuporomoka muda wowote.
Kwa mujibu wa wazazi wa shule hiyo, mazingira ya kusomea yamekuwa hatarishi mno, na hali hiyo inatishia kuathiri vibaya maendeleo ya wanafunzi kimasomo, huku baadhi yao wakilazimika kusomea nje, chini ya miti, bila miundombinu muhimu.
Wazazi wa shule hiyo wameeleza masikitiko yao, wakitoa wito kwa serikali kuu, serikali ya kaunti ya Turkana, pamoja na wahisani, kujitokeza kwa dharura ili kusaidia katika ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya.
Wanasema hatua hiyo itahakikisha usalama wa watoto na kuendeleza haki yao ya msingi ya kupata elimu bora katika mazingira salama.