Naibu Spika wa bunge la taifa Gladys Boss ameomba wadau wa masuala ya utawala kushirikiana katika kuhakikisha kwamba idadi ya wanawake wanaoshikilia nyadhifa muhimu za maamuzi inaongezeka.
Boss ambaye pia anawakilisha kaunti ya Uasin Gishu bungeni, alisema kwamba idadi ndogo ya wanawake katika nyadhifa za serikali ni suala la haki za kibinadamu.
Alisisitiza kwamba hali hiyo ina madhara makubwa sana katika jamii kwa sababu maoni ya jinsia ya kike hayazingatiwi inavyohitajika katika kufanya maamuzi.
“Wanawake ni karibu nusu ya idadi jumla ya watu nchini Kenya. Wakati mashirika ya utawala na hata sekta ya kibinafsi inakosa maoni ya nusu ya watu wote nchini, sote tunaumia.” alionya Boss.
Alikuwa akizungumza katika kikao za majadiliano ya kitaifa kuhusu uwakilishi wa kijinsia na uongozi kilichoandaliwa na chama cha mawakili wa kike nchini FIDA.
Mheshimiwa Gladys Boss alikuwa mgeni rasmi wa kikao hicho kilichohudhuriwa na wabunge wa kike kupitia chama chao cha KEWOPA na wabunge wa umri mdogo kupitia chama chao cha KYPA.
Kuhusu sheria ya thuluthi mbili ya uwakilishi, naibu huyo wa spika aliwasihi wabunge wa kike kuongoza harakati za kutafuta kupitishwa kwa sheria hiyo akisisitiza umuhimu wa sauti yao.