Wadau wa sekta ya haki waazimia kuimarisha vita dhidi ya ufisadi

Martin Mwanje
2 Min Read
Jaji Mkuu Martha Koome alipowaongoza wadau wengine katika kuzindua mkakati wa kupambana na ufisadi

Jaji Mkuu Martha Koome aliwaongoza wadau katika sekta ya haki katika kuzindua Mpangokazi Ongozi wa Kimkakati wa Kupambana na Ufisadi katika sekta hiyo humu nchini. 

Mpangokazi huo unalenga kukuza mfumo thabiti, wa uwazi na uwajibikaji wa sheria unaoangazia changamoto mbalimbali zinazosababishwa na zimwi la ufisadi.

 Wakati wa uzinduzi huo leo Jumanne, Jaji Koome alisisitiza kuwa mpangokazi huo utaziwezesha taasisi za sekta za haki kuelezea hatua bayana za kupambana na ufisadi, ikiwa ni pamoja na jitihada za muda mfupi, za muda wa kati na za muda mrefu za kupambana na jinamizi hilo.

“Kwa kukuza ushirikiano wa taasisi mbalimbali, tunaweza tukakabiliana vilivyo na ufisadi, kuboresha utoaji huduma na kurejesha matumaini katika taifa letu. Hii ni fursa ya kubadili hali ya mambo,” alisema Koome.

Aliongeza kuwa Baraza la Taifa la Sheria (NCAJ) limeelezea upya dhamira yake ya kuzuia na kukabiliana na ufisadi na uhalifu wa kiuchumi.

“Kama watu waliotwikwa majukumu, tunatambua kuwa mapambano dhidi ya ufisadi siyo tu suala la kisheria lakini la kimaadili. Ni wajibu wetu kulinda maadili ya taifa, kuhakikisha haki inadumu, na kuhamassisha maongozi ya wazi na uwajibikaji. Hatuwezi kamwe kuchukulia suala hili kama changamoto isiyoweza kukabiliwa, tunapaswa kuliona kama suala la dharura linalopaswa kuangaziwa,” alisisitiza Jaji Mkuu.

Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama Winfridah Mokaya kwa upande wake alitoa wito kwa wadau katika sekta ya haki kutoa mfano bora, kwa kuhakikisha kuwa haki inatolewa bila ushawishi wala upendeleo wowote.

Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula alisema Mpangokazi Ongozi wa Kimkakati wa Kupambana na Ufisadi wa Sekta ya Haki unalenga kuboresha namna sekta hiyo inavyokabiliana na ufisadi.

Website |  + posts
Share This Article