Wacha aende, asema Gavana Wanga kufuatia kujiuzulu kwa Naibu wake

Martin Mwanje
2 Min Read
Gavana Gladys Wanga (katikati) akiwa kwenye mkutano wa kisiasa

Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga amesema amekubali hatua ya Joseph Oyugi Magwanga kujiuzulu wadhifa wa Naibu Gavana wa kaunti hiyo.

Magwanga alitangaza kujiuzulu wadhifa huo akidai amehangaishwa vya kutosha katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Nakiri kupokea barua iliyoandikwa Februari 26, 2026 kutoka kwa Naibu Gavana akijiuzulu mara moja. Hii leo, nimekubali rasmi kujiuzulu kwake,” alisema Wanga ambaye pia kwenye taarifa ametangaza kiti hicho kuwa wazi kwa mujibu wa sheria.

Ameongeza kuwa wakati wakisubiri kuanza kwa mchakato wa kumsaka mrithi wa Magwanga kwa mujibu wa katiba, kipaumbele cha utawala wake ni kutoa huduma bora kwa wakazi wa Homa Bay.

Gavana Wanga na Magwanga wamegeuka kuwa mahasimu wa kisiasa licha ya kuchaguliwa pamoja katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Katika kujiuzulu, Magwanga ambaye ametangaza kuwa atagombea ugavana mwaka 2027, alisema ameshindwa kutoa huduma zake kutokana na vikwazo vilivyowekwa kwenye afisi yake.

Mathalan, anasema afisi yake ilifungwa mwezi Disemba mwaka jana, alipokonywa gari na lingine lilikosa kuwekwa mafuta.

Akiwahutubia wanahabari jana Alhamisi katika eneo la Oyugis, Kasipul, Magwanga alisema mazingira ya utendaji kazi hayamruhusu kutekeleza majukumu yake kikamilifu, hatua iliyomsababisha kujiuzulu badala ya kupokea mshahara bila kufanya lolote.

Inaaminika kuwa kinara wa zamani wa ODM hayati Raila Odinga alimshawishi Magwanga kutogombea Ugavana mwaka 2022 na badala yake kuwa Naibu Gavana wa Homa Bay.

 

Share This Article