Wabunge wataka mafuriko kutangazwa janga la kitaifa

Tom Mathinji
1 Min Read
Maeneo mengi ya nchi kushuhudia mvua kubwa.

Wabunge wa bunge la Taifa sasa wanamtaka Rais William Ruto kutangaza mafuriko kuwa janga la kitaifa na kuelekeza mikakati mwafaka ya kukabiliana na hali hiyo.

Wabunge hao waliahirisha shughuli za kawaida, kuelezea jinsi maeneo bunge yao yameathirika kutokana na mafuriko yanayosababishwa na mvua za El Nino.

Kulingana nao, kutangazwa kwa mafuriko hayo kuwa janga la kitaifa, kutavutia jumuiya ya kimataifa na wafadhili kuingilia kati na kuwasaidia wale ambao wameathirika.

Waziri wa Ulinzi  Aden Duale jana Jumanne alizuru  kaunti ya Mandera kama sehemu ya juhudi zinazoendelea za kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathiriwa wa mafuriko.

Mandera ni miongoni mwa kaunti za Kaskazini Mashariki mwa nchi ambazo zimeathirika na mafuriko kwa kiwango kikubwa.

Waziri alizuru mji wa  Elwak katika eneo la Mandera Kusini ambapo wakazi waliachwa bila makao kutokana na mafuriko.

Akiambatana na Gavana wa kaunti hiyo Mohamed Khalif, Duale alisema serikali kuu na zile za kaunti kaskazini mashariki mwa nchi zinafanya kila juhudi kutafuta suluhu mwafaka.

Share This Article