Zaidi ya Wawakilishi kumi wa Wanawake wamesema watapiga kura ya kuunga mkono kuondolewa mamlakani kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua siku ya Jumanne,katika bunge la taifa.
Wakiongozwa na Naibu spika wa Bunge la Taifa Gladys Shollei, wawakilishi hao walisema licha ya kwamba Naibu huyo wa Rais kuomba msamaha, bado watatekeleza haki yao ya kikatiba na baadaye watamsamehe.
Shollei ambaye mwakilishaji wa wanawake kaunti ya Uasin Gishu, alipinga madai kwamba hapaswi kuzungumzia swala la kuondolewa mamlakani kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa kuwa yeye ni naibu spika, akidokeza kuwa anazungumza kwa niaba ya watu wa Uasin Gishu.
Viongozi wengine wakiwemo mwakilishi wa Kaunti ya Migori, Fatuma Mohammed, Rahab Mukami (Nyandarua), Liza Chelule (Nakuru), Beatrice Kemei (Kericho), Rael Kasiwai (West Pokot), Jerusha Momanyi (Nyamira) na Rebecca Tonkei (Narok) walielezea kutoridhika kwao na miendendo ya Gachagua na kuapa kwamba watamtimua afisini leo Jumanne.
Wawakilishi hao wanawake walikuwa wakiongea katika uwanja wa Tonongoi, eneo bunge la Soin Sigowet, Kaunti ya Kericho, katika mkutano wa kuwawezesha wanawake almaarufu Wezesha Mama – Inua Jamii.