Wabunge wa kaunti ya Meru hasa maeneo yanayopakana na kaunti ya Isiolo, wamedhihirisha kutoridhika kwao kutokana na ongezeko la ukosefu wa usalama wakisema wizi wa mifugo umekuwa tatizo katika maeneo yao.
Wakizungumza huko Mikinduri wakati wa hafla ya kuchangisha pesa kusaidia kundi fulani la kina mama, wabunge hao Mpuru Aburi wa Tigania mashariki na John Mutunga wa Tigania Magharibi walilaumu maafisa wa polisi wakidai wanahusika kwenye wizi huo.
Wabunge hao sasa wanamtaka waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki aimarishe juhudi zake za kukabiliana na wizi wa mifugo.
Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula ambaye pia alihudhuria hafla hiyo ya mchango alisema kwamba wakenya wote wanastahili kuwa na usalama wa kutosha.
Wetangula aliitaka idara ya mahakama kutoa adhabu kali kwa wanaopatikana na makosa ya wizi wa mifugo akisema ndiyo njia pekee ya kukabiliana na uovu huo.