Wabunge katika Bunge la Taifa wamesisitiza dhamira yao ya kuokoa Hazina ya Taifa ya Ustawishaji wa Maeneo Bunge (NG-CDF) takriban mwaka mmoja kabla ya kuondolewa kwa hazina hiyo.
Mwaka jana, Mahakama Kuu ilitoa makataa ya NG-CDF kuacha kutumika mwezi Juni mwaka 2026.
Ni makataa hayo ambayo yalikuwa kiini cha mazungumzo wakati wa mkutano wa kikazi kati ya Kamati Teule ya Bunge la Taifa juu ya NG-CDF na Bodi na Usimamizi Mkuu wa NG-CDF.
Wazungumzaji wakati wa mkutano huo walitaja uamuzi wa hivi karibuni uliotolewa na Mahakama ya Juu, ambapo jopo la majaji saba wa mahakama hiyo lilibaini kuwa Sheria ya NG-CDF ya mwaka 2015 ilipitishwa kisheria.
Uamuzi huo ulihusu kesi iliyodumu muda mrefu iliyowasilshwa na Bunge la Seneti miaka 6 iliyopita kupinga sheria 23, ikiwemo sheria ya NG-CDF ya mwaka 2015.
Seneti iliwasilisha kesi hiyo ikidai haikuhusishwa na Bunge la Taifa katika upitishaji wake.
Miongoni mwa waliongumza kwenye mkutano huo ni Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge la Taifa juu ya NG-CDF ambaye pia ni mbunge wa Eldama Ravine Musa Sirma na mbunge wa zamani wa eneo bunge la Kisumu Mjini Magharibi Olago Aluoch ambaye kwa sasa anaongoza Bodi ya NG-CDF.
Wawili hao wakisema uamuzi wa Mahakama ya Juu utakuwa muhimu katika juhudi zinazoendelea za kuokoa hazina hiyo.
Wazungumzaji walisisitiza umuhimu mkubwa unaotekelezwa NG-CDF katika kukuza maendeleo mashinani na uwezeshaji wa raia.
“Hazina hiyo inasalia msingi wa maendeleo mashinani, ikiwezesha maeneo bunge kutekeleza miradi ya kuinua viwango vya maisha ya raia wetu,” alisema Sirma.
Wakati huohuo, Bunge la Taifa na Bodi ya NG-CDF zimekata rufaa dhidi ya uamuzi uliotolewa Septemba 20, 2024 ambapo jopo la majaji watatu liliitaja NG-CDF kuwa isiyokuwa ya kikatiba kwani inakiuka kanuni ya ugavi wa madaraka kati ya bunge na uongozi mkuu wa nchi.