Wabunge wa Gusii walalamikia unyanyasaji wa maafisa wa KNEC

Marion Bosire
2 Min Read

Wabunge kutoka eneo la Gusii sasa wanalalamikia kile wanachokitaja kuwa unyanyasaji unaotekelezwa na maafisa wa baraza la mitihani ya kitaifa KNEC dhidi ya watahiniwa wa mtihani unaoendelea wa kidato cha nne KCSE.

Viongozi hao wa kaunti za Kisii na Nyamira waliandaa kikao na wanahabari katika majengo ya bunge ambapo walisema kwamba unyanyasaji huo umeripotiwa kwenye kaunti zao.

Wakiongozwa na kiranja wa walio wengi katika bunge la taifa Sylvanus Osoro, wabunge hao walidai kwamba watahiniwa wa shule ya kitaifa ya wavulana ya Nyambaria katika kaunti ya Nyamira walishurutishwa kuvua nguo kabla ya kufanya mtihani.

Viongozi hao sasa wanataka kufahamu ni kwa nini eneo la Gusii limelengwa katika vitendo kama hivyo ambavyo wanasema vinajaza watahiniwa woga na huenda vikaathiri matokeo yao ya mtihani.

Haya yanajiri siku chache baada ya habari kusambaa kwamba mwalimu mkuu wa shule hiyo Bwana Charles Onyari ya Nyambaria alisimamishwa kazi kutokana na udanganyifu wa mtihani.

Alipokonywa pia jukumu la kusimamia kituo hicho cha mtihani wa kitaifa.

Shule hiyo ya Nyambaria ni mojawapo ya shule ambazo matokeo yake ya mtihani wa kitaifa yameimarika sana miaka ya hivi maajuzi.

Mwaka 2022 ilikuwa na alama wastani ya 10.89 ikilinganishwa na ya mwaka 2021 ambayo ilikuwa 9.31.

Waliopata alama ya A kwenye mtihani huo walikuwa 28, 383 wakapata alama ya A-, 76 wakapata alama ya B+ huku wa mwisho akipata alama ya B.

Share This Article