Tanzania imethibitisha kupokea rasmi taarifa kutoka kwa serikali ya Marekani kuhusu uamuzi wa kuiweka katika orodha ya nchi ambazo raia wake watatakiwa kuweka dhamana ya viza (visa bond) kabla ya kuingia nchini humo kwa madhumuni ya biashara (viza za B-1) au madhumuni ya utalii (viza za B-2).
Masharti hayo mapya yanatarajiwa kuanza kutekelezwa rasmi kuanzia Oktoba 23, 2025.
Hii inamaanisha kuanzia Oktoba 23, 2025, Watanzania na raia wa mataifa mengine kadhaa wanaoomba viza za B-1 (biashara) na B-2 (utalii) watatakiwa kuweka dhamana ya kuanzia dola 5000 za Marekani, sawa na shilingi 649,000 za Kenya, hadi dola 15,000 ambazo ni sawa na shilingi milioni 1.9 za Kenya ili wapewe fursa ya kuingia Marekani.
Tanzania imeingia kwenye orodha ya nchi za Afrika zilizowekewa sharti hilo, zikiwemo Malawi, Zambia, Gambia, Mali na Mauritania.
Uamuzi huo umefikiwa kufuatia utafiti uliofanywa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Marekani mwaka 2024, ambao ulitaja mataifa kadhaa kuwa na idadi kubwa ya watu ambao wakiingia Marekani wanapitiliza muda wa kukaa na wengine hufikia hatua ya kuzamia na kubakia Marekani licha ya viza zao kuisha.
Masharti haya mapya yana maana kuwa wale watakaorudi nchini mwao ndani ya muda sahihi watarudishiwa fedha zao wakirudi kwenye nchi zao, lakini wale watakaozidisha muda wa kukaa Marekani au kukiuka kanuni zozote za viza, pesa zao walizoweka dhamana hazitarudishwa.
Watu ambao watapewa viza chini ya masharti haya mapya watatakiwa kuingia Marekani na kuondoka kupitia uwanja wa ndege maalum ikiwemo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Boston Logan (BOS), ule wa John F Kennedy (JFK) na Washington Dulles (IAD), lengo likiwa ni kuweka urahisi wa ufuatiliaji wa utekelezwaji wa masharti mapya.