Makundi mawili ya waasi kutoka eneo la Darfur nchini Sudan, yanasema yatapigana pamoja na jeshi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Haya yanajiri baada ya wanajeshi wa (RSF) kupata mafanikio makubwa huko Darfur, ambako wameshutumiwa kwa mauaji ya kikabila.
Kiongozi wa waasi Gibril Ibrahim aliiambia BBC Newsday “wanataka kuwatetea raia wao” kutoka kwa RSF, ambayo anasema imekuwa ikiwazika watu wakiwa hai.
Alisema uamuzi wa kujiunga na jeshi si jambo rahisi.
Kiongozi wa vuguvugu la Justice and Equality Movement (Jem) alisema imechukua miezi saba kufikia muafaka.
Uhusiano kati ya Jem na jeshi la Sudan ni mgumu. Nduguye Bw Ibrahim aliuawa na jeshi, ambaye hapo awali alikuwa kiongozi wa kundi hilo.
Jem na Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan (SLM) walichukua silaha huko Darfur mwaka 2003, wakiishutumu serikali kwa kuzitenga jamii za Waafrika weusi wa eneo hilo.
Kisha serikali ilikusanya wanamgambo wa Kiarabu dhidi yao, na kusababisha kile ambacho kimetajwa kuwa mauaji ya halaiki ya kwanza ya Karne ya 21.
Wanamgambo hawa wamebadilika na kuwa RSF, ambayo imekuwa ikipigana na jeshi kwa udhibiti wa nchi tangu Aprili.
RSF imechukua miji kadhaa muhimu huko Darfur katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na jiji la pili kwa ukubwa nchini humo, Nyala.
Wiki iliyopita, kulikuwa na ripoti kwamba walikuwa wameua mamia ya watu katika mji mkuu wa Darfur Magharibi wa El Geneina.
RSF imekanusha kuhusika na mauaji hayo, ikisema ni sehemu ya “mzozo wa kikabila”.