Huduma ya taifa ya polisi imetoa onyo kali dhidi ya waandamanaji kuvamia majengo ya serikali.
Kupitia kwa taarifa Alhamisi alasiri, Inspekta jenerali wa polisi Japhet Koome amesema, licha ya kuwa wananchi wana haki ya kuandamana, huduma ya polisi haitawaruhusu kuvamia majengo ya serikali ikiwa ni pamoja na bunge, au kuvuruga vikao vya bunge.
“Huduma ya taifa ya polisi haitaruhusu waandamanaji kuvamia majengo yoyote ya serikali au kuvuruga vikao vya bunge,” alisema Koome kupitia kwa taarifa.
Matamshi ya Koome yanajiri huku maandamano yakiandaliwa kote nchini leo Alhamisi, kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024 ambao ulikuwa ukijadiliwa katika bunge la taifa.
Mswada huo ulipigiwa kura na kupita baada ya kusomwa kwa mara ya pili katika bunge la taifa, ambapo wabunge 204 walipiga kuunga mkono mswada huo, huku wabunge 115 wakiupinga.
Koome alisema huduma ya taifa ya polisi itaendelea kudumisha sheria, kulinda mali na maisha ya wananchi.