Mwanamuziki wa mtindo wa Dancehall Vybz Kartel sasa yuko huru baada ya mahakama ya rufaa kukataa kuanzisha upya kesi ya mauaji dhidi yake.
Mwaka 2014, Kartel alipatikana na hatia ya kumuua Clive “Lizard” Williams, uamuzi uliobatilishwa mapema mwaka huu.
Jana Jumatano Julai 31, 2024, mahakama ya rufaa nchini Jamaica ilikataa kuanzisha upya kesi hiyo hiyo ya mauaji na hivyo sasa yuko huru.
Mwezi Machi mahakama ilipata ushahidi wa utovu wa maadili kwa upande wa waamuzi wa kesi ilipokuwa ikiendelea awali.
Baada ya kugundua hilo, baraza la washauri la Uingereza liliachia jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufaa nchini Jamaica kuamua iwapo wataanzisha kesi hiyo upya au watamwachilia huru Vybz na washtakiwa wenza.
Kesi dhidi ya Kartel na washtakiwa wenza iliendeshwa kwa muda wa miezi miwili hivi kabla ya kupatikana na hatia Machi 14, 2014.
Waendesha mashtaka walidai kwamba Williams aliuawa kwa sababu ya bunduki zilizokuwa zimetoweka na kwamba Kartel alimhadaa akaja nyumbani kwake ambapo alipigwa hadi akafa.
Polisi wa Jamaica walitoa ushahidi mahakamani wakidai kwamba waliona ujumbe kwenye rununu ya Kartel ulisema kwamba ‘mwili Williams uligeuzwa nyama ya kusaga.
Kadhalika mwili wa Williams haukuwahi kupatikana .
Kesi ilipokuwa ikiendelea, mmoja wa waamuzi alilaumiwa kwa kile kilochotajwa kuwa kuwapa hongo waamuzi wengine na hata baada ya kufahamishwa, jaji akaamua kuendelea na kesi badala ya kuisimamisha.
Madai ya kuhongwa kwa waamuzi wa kesi hiyo yamekuwa msingi wa utetezi wa Kartel katika rufaa yake ya miaka mingi.
Kartel alikuwa mmoja wa wasanii wakubwa wa muziki nchini Jamaica alipopatikana na hatia.
Amewahi kushirikiana na wasanii tajika kama Rihanna, Missy Elliot, Busta Rhymes na Pitbull.
Aliendelea kitayarisha muziki akiwa kizuizini.