Vurugu zilizotokea jana usiku katika jiji kuu la kibiashara la Tanzania Dar es Salaam, zinaripotiwa kusababisha uharibifu hali ambayo imesababisha maafisa kadhaa kuchukuliwa hatua.
Jumanne Muliro ambaye ni kamanda wa polisi huko Dar es Salaam, alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo ambapo mabasi ya mwendokasi almaarufu BRT yaliharibiwa pamoja na vituo vinne vya mabasi hayo.
Mabasi na vituo hivyo vilipigwa kwa mawe na wananchi waliokuwa wakilalamikia changamoto mbalimbali.Vurugu za watu hao ziligusa hata vituo vya polisi vya Magomeni Usalama na Magomeni Kagera, ambavyo viliharibiwa.
Muliro alieleza kwamba maafisa wa polisi walifika haraka katika maeneo husika na kudhibiti hali hiyo, hasa eneo la Kagera, ambapo mabasi ya mwendokasi yalikuwa yakielekea Ubungo hadi Kimara.
Kamanda Muliro alikumbusha wananchi kwamba ni makosa kisheria kufanya uharibifu wa mali ya umma, hususan miundombinu ya usafiri kama mabasi ya mwendokasi.
Polisi wanaendeleza uchunguzi wa tukio hilo la usiku wa kuamkia leo ambapo washukiwa watatu wanaripotiwa kutiwa mbaroni huku Rais Samia akiwasimamisha kazi maafisa kadhaa wa mabasi ya mwendokasi.