Idara ya utabiri wa hali ya hewa hapa nchini imewashauri wakenya kujiandaa kukabiliana na viwango vya juu vya joto katika sehemu mbali hapa nchini kuanzia leo Jumanne.
Imetabiriwa kwamba kuanzia leo Jumanne, Februari 20 hadi Februari 26, viwango vya juu vya joto vitakuwa zaidi ya nyuzi 30 katika kaunti za Turkana, Samburu, Marsabit, Mandera, Wajir, Isiolo, Garissa na Tana River.
Kupitia taarifa, mkurugenzi wa idara hiyo David Gikungu amesema kaunti za Lamu, Kilifi, Mombasa, Kwale, Taita Taveta, Kajiado, Makueni, Kitui, Machakos, Nairobi, Kiambu, Embu, Laikipia, Elgeyo-Marakwet, Pokot Magharibi, Bungoma, Kakamega, Busia, Narok na Baringo, pia zitashuhudia viwango vya juu vya joto vya zaidi ya nyuzi 30.
Hata hivyo baadhi ya maeneo katika kaunti za Meru, Tharaka Nithi, Murang’a, Nyeri, Nyandarua, Nakuru, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia, na West Pokot yanatazamiwa kushuhudia viwango vya juu vya joto vya chini ya nyuzi 25.
Gikungu amewataka wakenya kunywa maji mengi na kuchukua tahadhari dhidi ya miale ya jua katika siku ambazo jua litakuwa kali na pia akiwashauri kuvalia mavazi yenye joto wakati wa baridi nyakati za usiku.
Taifa limekuwa likishuhudia ongezeko la kiwango vya joto mchana na usiku.