Vivutio tisa vya utalii vyazinduliwa hapa nchini

Tom Mathinji
2 Min Read
Vivutio tisa vya Utalii vyazinduliwa hapa nchini.

Sekta ya utalii hapa nchini, inatarajiwa kuimarika zaidi baada ya kuzinduliwa kwa vivutio tisa vya kitalii, vinavyo kusudiwa kupiga jeki utalii wa ndani ya nchi.

Vivutio hivyo vilizinduliwa na wizara ya utalii na huduma za wanyamapori, chini ya mpango wa Tembea Kenya kama sehemu ya kuboresha utalii kwa kuonyesha vito fiche.

Akizungumza katika Kaunti ya Kisumu, waziri wa utalii na Wanyamapori Rebecca Miano,  alisema hatua hiyo inanuiwa kuimarisha sekta ya utalii nchini, kukidhi mahitaji ya sasa huku pia juhudi za uhifadhi mazingira zikitekelezwa.

“Tumejumuisha maswala kama vile matukio, michezo, utamaduni, utalii wa kiafya na kimazingira miongoni mwa mengine. Kila eneo lina kivutio, na tunawahimiza wageni kuzuru maeneo hayo,” alisema Miano.

Kama sehemu ya juhudi hizo, wizara hiyo pia imezundua mashindano ya upigaji picha, ili kuwapa motisha wakenya kuonyesha vivutio bora katika maeneo wanakotoka.

Kwa upande wake, Gavana wa Kaunti ya Narok Patrick Ole Ntutu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Baraza la Magavana ya Utalii na Wanyamapori, alihimiza serikali iongeze mgao kwa utalii.

Ntutu alisema Utalii ukitumika vizuri unaweza kuchangia katika ongezeko la pato la Taifa na kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana. 

Serikali imeondoa ada za viingilio kwa wananchi wanaotembelea  hifadhi za taifa kesho ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya utalii duniani.

TAGGED:
Share This Article