Vivianne Ke asema familia yake ilimtesa alipokuwa akipitia talaka

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Vivianne Ke jana alichapisha kwenye mitandao ya kijamii taarifa kuhusu jinsi watu wa familia yake walimtesa na kumtelekeza alipokuwa anapitia talaka.

Alisema wakati huo dadake alimtaja kuwa mtu ambaye ana matatizo ya kiakili huku shangazi yake akikwenda kumnyanyasa katika makazi yake.

“Nilipojaribu kurejea nyumbani kutoka magharibi, mamangu aliniuliza ni kwa nini.” aliandika mwanamuziki huyo ambaye sasa anaishi nchini Marekani.

Kulingana naye, aliibua kiwewe ambacho kimeghubika familia yake kwa vizazi kadhaa, hali aliyorejelea kuwa laana ambayo inajirudia katika kizazi kinachokua cha familia yake.

“Wanawake katika ukoo wa mamangu wamekufa ganzi wakiongozwa na dadangu.” aliendelea kusema Vivianne akiongeza kusema kwamba hawawezi kumnyamazisha au kumvunja.

Aliahidi kuendelea kupaaza sauti kwa niaba yake binafsi na kwa niaba ya watoto wake kwa sasabu kunyamazishwa, kurushiwa woga, unyanyasaji na ubinafsi ni lazima vikome.

Leo tena ameandika ujumbe mwingine akisema kwamba maneno aliyochapisha jana yanaonekana kuwakera watu wa familia yake ambao wanamrushia maneno ya kila aina.

“Kabla hatujavurugika, kila kitu nilichosema jana ni ukweli. Labda wengi wamepitia suala kama hilo. Aibu, kutengwa na maumivu ya kihisia ambayo tunapitia katika familia zetu lazima yaponywe.” ameandika mwimbaji huyo.

Anashangaa tabia ya kufanya uraibu na mawasiliano duni kuwa jambo la kawaida kutaendelea hadi lini huku akitambua kwamba yeye sio mkamilifu lakini huwa anajaribu.

Mama huyo wa binti mmoja anasema hakustahili kutelekezwa alipokuwa akipitia magumu akisisitiza kwamba wanafamilia ni lazima wapendane na kusaidiana.

Vivianne alikuwa kwenye ndoa na mfanyabiashara Sam West na uhusiano wao wa kimapenzi ulifahamika baada yake kumchumbia Vivianne mubashara kwenye runinga mwaka 2017.

Ndoa yao ilivunjika kimya kimya na Vivianne akahamia Marekani.

Website |  + posts
Share This Article