Katibu wa uhamiaji Julius Bitok amesema kwamba vitambulisho vipya almaarufu Maisha Card vimechapishwa ambapo kufikia sasa idadi ya vitambulisho hivyo vilivyo tayari ni 505,197.
Kati ya vitambulisho hivyo vilivyochapishwa katika muda wa siku 14 zilizopita, 162,856 ni vya wanaochukua vitambulisho kwa mara ya kwanza kabisa huku 344, 341 vikiwa vya waliokuwa na vitambulisho na wakatuma maombi ya vingine kwa sababu labda vilipotea au kuharibika.
Maombi yanayoshughulikiwa kwa sasa ya vitambulisho ni 1,358 pekee kulingana na Bitok.
Bitok amefafanua kwamba afisi ya usajili wa watu nchini imeondoa mrundiko uliokuwepo wa maombi ya vitambulisho na sasa inachapisha haraka vitambulisho vya maombi mapya.
Anasema afisi hiyo sasa inachapisha hadi vitambulisho elfu 32,000 kwa siku huku akihimiza waliokuwa wametuma maombi ya vitambulisho waende kuvichukua.
Kufikia jana jioni, Bitok anasema kulikuwa na vitambulisho 476,167 ambavyo havikuwa vimechukuliwa kwenye vituo mbali mbali nchini vya afisi ya usajili wa watu na vituo vya Huduma.
Kaunti ya Nairobi inaongoza katika idadi ya vitambulisho ambavyo havijachukuliwa ambavyo ni elfu 55,327, inafuatiwa na Kiambu ambapo vitambulisho elfu 37,708 vimechapishwa vikisubiri kuchukuliwa na wenyewe.
Serikali ilianza kuchapisha vitambulisho hivyo vipya aina ya Maisha Card baada ya mahakama kuu kuondoa agizo ililokuwa imetoa la kusitisha uchapishaji.
Agosti 12, 2024, Jaji Lawrence Mugambi alitangaza kuondolewa kwa maagizo yaliyozuia utekelezaji wa Maisha Card.