Wizara ya Afya imethibitisha kupitia taarifa, kugunduliwa kwa visa vitatu zaidi vya ugonjwa wa Mpox nchini Kenya.
Visa hivyo viligunduliwa katika kaunti za Mombasa, Nakuru na Nairobi na vinafikisha idadi jumla ya visa nchini kuwa 17.
Wizara ya Afya ilipongeza wananchi kwa kuzingatia kanuni za kujikinga na ugonjwa huo hatua inayosemekana kupunguza pakubwa maambukizi.
Katika kaunti za Nakuru visa vilivyogunduliwa ni vitatu, Kajiado na Bungoma viwili kila mija na kisa kimoja kimoja katika kaunti za Taita Taveta, Busia, Makueni, Kericho, Uasin Gishu na Kilifi.
Wagonjwa watatu wako chini ya uangalizi wa madaktari, 13 wamepona kabisa na kifo kimoja kimeripotiwa.
Huku ikisisitiza umuhimu wa kufuatilia waliotagusana na wagonjwa wizara ya Afya inasema watu 83 wametambuliwa na 78 kati yao wamekamilisha kipindi cha siku 21 cha ufuatiliaji.
Wawili wako chini ya uangalizi wa madaktari na wasafiri 15,068 wamepimwa katika viingilio mbali mbali vya nchi hii.
Wakenya wanashauriwa kutokwenda safari zisizo za lazima hadi maeneo yaliyoathiriwa na uginjwa wa Mpoxwizara inapotafuta mbinu za kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo kwa ajili ya wakazi wa maeneo yaliyoathirika.
Waziri wa Afya Deborah M. Barasa amewataka wakenya kusalia macho na kuzingatia kanuni za kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kama vile kutotangamana na wagonjwa, kudhibiti idadi ya wapenzina kuzingatia usafi.
Ili kupata usadizi kwa wanaoshuku kuambukiwa Mpox wanashauriwa kufika katika kituo cha afya kilicho karibu haraka na wanaweza kupiga simu nambari, 719, 0729 471 414 na 0732 353 535.
“Tunapofuatilia hali hii, ni muhimu tushirikiane kuzuia maambukizi ya Mpox.” alisema Waziri Barasa.