Vipusa wa Kenya wapigwa laza na Uingereza Kombe la Dunia

Dismas Otuke
1 Min Read

Kenya ilianza vibaya makala ya nane ya fainali za Kombe la Dunia kwa wasichana walio chini ya umri wa miaka 17 mapema leo, baada ya kupigwa na Uingereza mabao 2-0 katika kundi C.

Pambano hilo lilipigwa katika uga wa Cibao mjini Santiago katika Jamhuri ya Dominica.

Kenya wanaonolewa na Mildred Cheche, walianza vyema mchuano huo wakijihami vyema hadi dakika ya 29,  wakati Uingereza ilifunga kupitia penati ya Lola Brown na kipindi cha kwanza kumalizika  hivyo.

Junior Starlets walirejea awamu ya pili wakijaribu kwa udi na uvumba kukomboa goli hilo,ila kipusa bahati alikosa kutabasamu na badala yake makosa ya mabeki yakamruhusu Lauryn Thompson kuongeza la pili dakika ya 87.

Kenya itarejea uwanjani Jumapili usiku kwa mchuano wa pili dhidi ya Korea Kaskazini, ambao walishinda mechi yao ya ufunguzi mabao 3-1 dhidi ya Mexico.

Mchuano wa mwisho wa makundi kwa Junior Starlets ambayo ni timu ya kwanza ya Kenya kufuzu kwa Kombe la Dunia ,utachezwa tarehe 24 mwezi huu dhidi ya Mexico.

Matokeo ya Kombe la Dunia ya jana

 

Share This Article