Viongozi katika eneo la magharibi wameahidi kuendelea kufanya kazi na serikali jumuishi.
Walitoa ahadi hiyo wakati ziara ya siku nne ya Rais William Ruto eneo hilo ikiingia siku ya pili leo Ijumaa.
Viongozi wengi waliotoa ahadi hiyo ni wanachama chama cha ODM, ambacho kiongozi wake Raila Odinga alifariki Oktoba 15 wakati akipokea matibabu nchini India.
Eneo la magharibi lilikuwa ngome ya kisiasa ya Raila miaka nenda miaka rudi.
Viongozi hao wakisema kuwa Raila alichukua hatua ya kijasiri kuunganisha upinzani na serikali kwa ajili ya umoja wa taifa na mabadiliko jumuishi ya kitaifa.
Waliyasema hayo katika maeneo mbalimbali wakati wa ziara ya maendeleo ya Rais Ruto katika kaunti ya Busia.
Gavana wa kaunti hiyo Dkt. Paul Otwoma alisema viongozi kutoka upinzani na serikalini wataendelea kufanya kazi pamoja kuharakisha maendeleo kuendana na matamanio ya Raila.
Alimpongeza Rais Ruto akisema ameonyesha dhamira ya kuyatumikia maeneo yote na kurejelea rekodi ya maendeleo ya serikali katika kaunti hiyo.
“Tulikuwa kwenye kambi tofauti! Tulikuwa kwenye kambi ya Bw. Odinga. Hata hivyo, Odinga aliungana na Rais Ruto. Kwa bahati mbaya, alituacha, lakini alituacha serikalini,” aliongeza Dkt. Otuoma.
Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, ambaye pia ni naibu kiongozi wa zamani wa ODM, alisema wanachama wa chama hicho wameazimia kusalia katika serikali jumuishi walikoachwa na Raila.
“Kwa miaka 13, nilikuwa naibu wa Bw. Odinga. Alituacha na Rais Ruto. Kwa hivyo tutafanya kazi kuelekea kutimiza alichokubaliana na Rais Ruto – kuiunganisha nchi,” aliongeza Gavana huyo wa zamani wa Kakamega.
Matamshi sawia yalitolewa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi aliyesema Rais Ruto na Raila waliunda serikali jumuishi ili kuiunganisha nchi.
Alitoa wito kwa Wakenya kuepukana na makundi madogo na yenye kuleta migawanyiko ya kisiasa na badala yake kuungana na kuendeleza ajenda ya maendeleo nchini.
“Tusiondoke kwenye meli kubwa na kuingia kwenye boti ndogo wakati kukiwa na mawimbi makubwa,” alishauri Mudavadi.
Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula alitoa wito wa umoja na kuwataka viongozi kutumia serikali jumuishi kufanya kazi kuelekea lengo moja.
Alisema wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, kulikuwa na kambi mbili kuu za kisiasa: Kenya Kwanza na Azimio la Umoja, ambazo sasa zimeungana.
“Kama jamii na watu wa eneo hili, hebu tuungane na kumuunga mkono Rais wetu, kukuza amani katika taifa letu ili maendeleo yaweze kumfikia kila mtu. Hebu tuwakatae wale wanaoneza siasa za chuki na hisa. Hawana ajenda mbali na kaulimbiu ‘Ruto must go’,” alisema Wetang’ula.