Mbio za marathon za maadhimisho ya 52 ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya mkuu wa majeshi nchini Uganda Muhoozi Kainerugaba, zitaandaliwa Aprili 26, 2026 katika uwanja wa Kololo jijini Kampala.
Waandalizi wa mbio hizo wakiongozwa na mkurugenzi wa kituo cha habari cha Uganda Allan Kasujja waliandaa kikao na wanahabari jana kutangaza ujio wa mbio hizo.
Kasujja alielezea kwamba maushui ya mwaka huu ya mbio hizo ni “Kimbia kwa ajili ya hisani, kimbia kwa ajili ya tumaini” huku akialika raia wote wa Uganda kushiriki.
Alielezea kwamba pesa zote zitakazokusanywa kutokana na mbio hizo zitaelekezwa katika kusaidia watoto yatima katika sehemu mbali mbal za Uganda.
Mkurugenzi huyo wa kituo cha habari cha Uganda alimsifia Jenerali Muhoozi kwa ukarimu wake akisema kwamba badala yake kuandaa sherehe ya faragha na watu wake wa karibu, ameamua kushiriki siku hiyo muhimu na wananchi.
Suala lingine alilofafanua Kasujja ni kwamba mbio hizo hazihusu wanaounga serikali mkono pekee bali ni za kila raia wa Uganda bila kuangazia miegemeo ya kisiasa.
Mwaka jana, Kainerugaba aliandaa mbio sawia ambazo ziliongozwa na maudhui ya mabadiliko ya tabianchi ambapo waandalizi walitaka kuhamasisha umma kuhusu jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.
Muhoozi Kainerugaba ni mwanawe Rais Yoweri Museveni aliyezaliwa Aprili 24 1974. Anahudumu kama mkuu wa majeshi nchini Uganda kando na kuwa mwenyekiti wa chama cha wazalendo cha Uganda.