Viongozi wa jamii ya Wasomali katika kaunti ya Isiolo wamemshtumu Waziri wa Usalama wa Kitaifa Prof. Kithure Kindiki kwa madai ya kukosa kuchukua hatua wakati visa vya ukosefu wa usalama eneo hilo vikiongezeka.
Wanasema visa hivyo vimesababisha vifo na kupotea kwa mali katika eneo hilo na sasa wanamtaka Rais William Ruto kuingilia kali ili kudhibiti hali hiyo.
Wakiwahutubia wanahabari, viongozi hao wakiongozwa na Katibu Mkuu wao Idle Hassan walisema visa vya wizi wa mifugo vinaongezeka licha ya ziara za mara kwa mara zilizofanywa ka Prof. Kindiki eneo hilo.
Kulingana nao, Prof. Kindiki ameishia kutoa tu vitisho kwa wahalifu kwamba operesheni ya usalama itafanywa eneo hilo kuwafurusha lakini hatua haijachukuliwa na serikali kuwarejesha mifugo walioibwa na kuwafurusha wahalifu hao hadi kufikia sasa.
Matamshi yao yanakuja siku moja baada ya Rais William Ruto juzi Jumamosi kufanya mkutano na wasimamizi wakuu wa usalama nchini kuhusu hali katika eneo la North Rift ambapo alifahamishwa kuhusu inavyoendelea “Operation Maliza Uhalifu”.
Wakati wa mkutano huo, Ruto alisema kwamba utulivu umerejea katika eneo la kaskazini mwa bonde la ufa kufuatia operesheni ya kiusalama iliyoanzishwa eneo hilo mwaka mmoja uliopita.
Aliongeza kwamba visa vya hivi majuzi vya ujambazi na wizi wa mifugo katika eneo hilo vinashughulikiwa na maafisa wa usalama ambao wanatumia mbinu mpya.
“Tumejitolea kuhakikisha amani na usalama vinarejea katika eneo la North Rift na sehemu nyingine za nchi ambazo zimeshuhudia kuvurugwa kwa amani na usalama,” alisema Rais.
Aliyasema haya baada ya mkutano na wasimamizi wakuu wa usalama nchini kuhusu hali katika eneo la North Rift ambapo alifahamishwa kuhusu inavyoendelea “Operation Maliza Uhalifu”.