Spika wa bunge Moses Wetangula kwa mara nyingine amehimiza viongozi wa eneo la Magharibi kuwa na umoja akisisitiza kwamba maazimio ya maendeleo katika eneo hilo yanategemea pakubwa umoja huo.
Wetangula alitaja uwezo mkubwa wa kimaendeleo wa eneo hilo ambao anasema unasubiri ushirikiano wao ili kuafikiwa na kwamba umoja unaweza kusababisha makubwa.
Aliwashauri kujitenga na viongozi wa kisiasa ambao wanaeneza siasa za migawanyiko akiongeza kwamba wakati umewadia kwa eneo la Magharibi kutumia ushawishi wake mkubwa katika siasa za kitaifa.
Spika Wetangula alikuwa akizungumza jana alipohudhuria hafla ya kuchangisha pesa za kusaidia makundi ya kina mama katika eneo bunge la Sabatia kufuatia mwaliko wa mbunge wa eneo hilo Clement Sloya.
Alisema ni bayana kwamba kuwezesha wanawake kwa namna yoyote ile ni sawa na kuwezesha familia nzima, jamii nzima na hatimaye kuwa na mataifa bora.
Mchango wa pamoja wa Wetangula, Rais William Ruto na waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi,kwenye hafla hiyo ya jana ni shilingi milioni 3.
Wetangula alikuwa ameandamana na msaidizi wa Rais Ruto Farouk Kibet, wabunge John Waluke wa Sirisia, Nabii Nabwera wa Lugari, David Ochieng’ wa Ugenya, Samson Cherargey seneta wa Nandi, Malulu Injendi wa Malav), Beatrice Adagala wa kaunti ya Vihiga, Majimbo Kalasinga wa Kabuchai na Dick Maungu wa Luanda kati ya wengine wengi.